Tuesday , 31st Mar , 2015

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete jana amehutubia katika kongamano la siku tatu kuhusu mikakati mipya ili kutokomeza ukosefu wa ajira, linalofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York.

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete akihutubia katika kongamano la siku tatu kuhusu mikakati mipya ili kutokomeza ukosefu wa ajira,

Amesema nchi za kiafrika zimezalisha ajira milioni 37 kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, wakati kila mwaka ni vijana milioni 122 ambao wanaingia kwenye soko la kazi, akisema hiyo ni changamoto.

Rais Kikwete amesema, ingawa amefurahi kuona kwamba ukosefu wa ajira umewekwa kipaumbele na jamii ya kimataifa hadi kuwa moja ya malengo ya maendeleo endelevu, bado nusu ya wafanyakazi duniani kote wanakumbwa na hali ngumu ya ajira, na wamekosa ruzuku ya serikali.

Aidha rais wa Tanzania amesema ni changamoto kwamba ukosefu wa ajira bora unaweza kuwa hatari kwa mshikamano wa jamii na hatimaye usalama wa nchi, huku akitaja vikundi vya kigaidi vinavyotumikisha vijana ambao hawana kazi.

Mkutano huo ambao umeandaliwa na Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC na Shirika la Kazi Duniani ILO utamulika hali ya wafanyakazi wengi duniani ambao wanakumbwa na hali ngumu ya maisha, wakiwa na kazi zisizo kuwa rasmi, mishahara midogo au kazi zisizokuwa imara.