
Mshambuliaji Malimi Busungu aliyesajiliwa na Yanga
Katika taarifa yake, Katibu wa Yanga SC, Dk Jonas Tiboroha amesema wamemalizana na Busungu ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuhamia kikazi Yanga SC.
Busungu amekuwa mchezaji tegemeo wa Mgambo JKT kwa misimu mitatu na wiki hii aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Kwa upande wa Mbeya City imefanikiwa kumnasa beki wa zamani wa Simba, Haruna Shamte pamoja na kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Joseph Maundi.
Shamte ambaye misimu miwili iliyopita amekuwa akiitumikia JKT Ruvu, amesaini mkataba wa mwaka mmoja huku Maundi akisaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu kwa ajili ya kukitumikia kikosi hicho katika msimu ujao wa Ligi kuu Soka Tanzania Bara.