Jumanne , 5th Mei , 2015

Uchaguzi wa chama cha mpira wa vinyoya nchini TBA uliokuwa ufanyike Mei tatu mwaka huu umepelekwa mbele mpaka Mei 16 mwaka huu kutokana na idadi ndogo ya wagombea kujitokeza.

Akizungumza na East Africa Radio, afisa habari wa baraza la michezo nchini BMT, Najaha Bakari amesema, uchaguzi huo umekuwa na matatizo kidogo kwani hapo awali uchaguzi huo ulitakiwa ufanyike April 25 lakini ulipelekwa mbele mpaka Mei tatu kutokana na wagombea wa nafasi mbalimbali katika chama hicho kuchukua fomu lakini hawakurudisha fomu hizo.

Najaha amesema, wagombea wote wa nafasi mbalimbali wamepewa muda wa kuchukua fomu ambapo mpaka Mei 15 zoezi la kuchukua na kurudisha fomu litakuwa limekamilika kwa ajili ya kufanya uchaguzi Mei 16 mwaka huu.

Najaha amesema fomu za ugombea zilichukuliwa saba lakini zilizorudishwa ni nne ambazo ni ya nafasi moja ya mwenyekiti, katibu mkuu na wajumbe wawili.

Najaha amesema, mpaka ikifika muda uliopangwa kwa ajili ya uchaguzi huo na hakuna waliojitokeza hawataweza kuahirisha na wapiga kura watapiga kura za ndiyo na hapo baadaye watafanya uchaguzi mdogo kwa ajili ya kupata viongozi wengine wa chama hicho.