Jumanne , 21st Apr , 2015

Serikali ya Tanzania imeshauriwa kuweka mazingira bora ya ajira kwa vijana ili kuepukana na tatizo la vijana wengi kuondoka hapa nchini kwenda nchi za nje kwa ajili ya kutafuta ajira.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa umma nchini Tanzania, Hashim Rungwe (kulia), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa umma nchini Bw, Hashim Rungwe amesema serikali imeshindwa kuwa na sera nzuri za ajira kwa vijana, ndio sababu inayopelekea vijana kukimbilia nchi za nje ikiwemo Afrika Kusini kwa ajili ya kutafuta ajira.

Amesema iwapo serikali itaendelea na mfumo wake wa kutowawekea vijana mazingira bora ya ajira kuna hatari ya vijana wenyewe kuendelea kukimbilia nje ya nchi kutafuta ajira kwa nguvu huku wakielewa kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria za nchi husika.

Wakati huo huo, Mashirika na taasisi binafsi na umma nchini Tanzania, yametakiwa kushirikiana na serikali katika kuwajenga vijana wawe wazalendo na wanaoipenda nchi yao, ili kuepusha kukithiri kwa rushwa pamoja na tabia iliyoanza hivi sasa ya vijana wengi kutaka kujiunga na vikundi vya kigaidi.

Afisa kutoka taasisi inayojishughulisha na uelimishaji umma kuhusu uzalendo ya Tanzania Zalendo Bw. Sikhi Ramadhani Magoha, amesema hayo leo ambapo amezishauri kampuni zinazojihusisha na biashara ziwe za kwanza kuunga mkono juhudi hizo za serikali, kwani mahali pasipo na amani kamwe biashara nazo haziwezi kustawi.

Magoha ametaja maeneo ambako kampuni zinaweza kuwajenga vijana kuwa wazalendo kuwa ni pamoja na kuwapatia ajira, kuwakutanisha pamoja katika mijadala ya namna ya kutambua umuhimu wao katika jamii ili watumike ipasavyo katika kuilinda na kuijenga nchi yao.