Mwili wa Mtanzania Joshua Mollel, aliyeuawa na kundi la Hamas nchini Israel miaka miwili iliyopita, utawasili leo, Novemba 19 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ukitokea Tel Aviv, Israel.
Hatua hii inafuatia makabidhiano yanayoendelea kufanyika kati ya nchi ya Israel na Kundi la Hamas kutoka Palestina.
Israel imepokea miili ya mateka 19 Waisraeli waliorejeshwa na Hamas, pamoja na miili ya mateka watatu raia wa kigeni,raia mmoja wa Thailand, mmoja wa Nepal na Mtanzania mmoja.
Kwa upande mwingine, imekabidhi jumla ya miili 285 ya Wapalestina ikiwa ni sehemu ya makubaliano hayo yaliyopelekea kutamatika kwa vita hivyo.
Ibada maalumu ya kumuaga marehemu ilifanywa na Ubalozi wa Tanzania nchini Israel siku ya jana Jumanne, Novemba 18 kabla ya safari ya kurejeshwa nchini.
Mollel alikuwa akifanya mafunzo ya kilimo katika eneo la Kusini mwa Israel, kabla ya mashambulizi ya ghafla ya Hamas ya Oktoba 7,2023 nchini Israel yaliyoua watu 1,205 na wengine zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka na kusababisha vita vilivyodumu kwa miaka miwili na vifo vya zaidi ya Wapalestina 67,000.
