Ijumaa , 2nd Mei , 2025

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetangaza kitaanzisha kamati maalum itakayoratibu mpango wa kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya kisheria, haki za binadamu na utawala bora.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) , Boniface Mwabukusi

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 2, 2025 na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) , Boniface Mwabukusi jijini Dar es Salaam na kusema kuwa kamati itakayoundwa itajumuisha viongozi waandamizi wastaafu wa Serikali, wakiwemo mawaziri na wazee mashuhuri waliowahi kulitumikia Taifa katika nafasi mbalimbali.

"Tunatarajia kuomba wazee wetu, 'states people' ambao tunao katika Taifa letu, tuonane na Amiri Jeshi Mkuu ili kuzungumza naye kuhusu haya yanayoendelea na nini TLS tunashauri," amesema Rais wa TLS

Akizungumzia tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima, Mwabukusi amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wanawachukulia hatua stahiki wale wote waliohusika na tukio hilo Kwani ni la kikatili.

Aidha akizungumzia tukio lililotokea katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam Aprili 24, siku ambayo Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu alitakiwa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi yake ya uhaini Mwabukusi amesema kuwa kitendo hicho si cha kiungwana na TLS wanakilaani kwa nguvu zote.