Jumatano , 26th Feb , 2025

Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mwanga Lembrus Mchome, amemuomba Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika, kujibu barua yake ya malalamiko ya kupinga uteuzi wa viongozi nane wa CHADEMA walioteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu Januari 22, 2025.

Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mwanga Lembrus Mchome

Miongoni mwa viongozi anaopinga uteuzi wao ni pamoja na Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar pamoja na wajumbe watano wa kamati kuu akiwemo Godbless Lema akidai kuwa uteuzi wa viongozi huo ulikiuka katiba ya chama hicho.

Mchome amesema katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba KM/CDM/AD/2025 ilitaka ufafanuzi wa uhalali wa viongozi hao kupitishwa na akidi ndogo ya wajumbe.

Kwa mujibu wa Mchome, amesema kuwa akidi ya Baraza Kuu la CHADEMA wajumbe wake ni wanachama 412 ambayo akidi inayotakiwa angalau iwe na wajumbe 309 sawa na asilimia 75 lakini viongozi hao walipitishwa na akidi ya wanachama 85 tu sawa na asilimia 20.6.