Jumanne , 25th Feb , 2025

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar amesema hataki uhusiano wa nchi yake na Ulaya ushikiliwe mateka kutokana na mitazamo ya watu kuhusu mzozo kati ya Israel na Hamas.

Kauli yake ameitoa wakati Israel imeanza tena mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuhusu mustakabali wa Gaza iliyoharibiwa na vita.

Saar amefanya mazungumzo na maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels huku EU ikitafakari kuchukua jukumu katika ujenzi mpya wa Gaza baada ya makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano mwezi uliopita.
Soma pia: Israel yasema itachelewesha zoezi la kuwaachia wafungwa wa Kipalestina 

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Israel ameshiriki mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Israel akiwa pamoja na mkuu wa sera za kigeni wa EU Kaja Kallas, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika tangu mwaka 2022.

Kallas amesema kikao hicho kilikuwa cha "wazi”, akiuambia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari kwamba, amefurahi kushiriki.

Mkuu huyo wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali katika ukanda wa Gaza na eneo la Ukingo wa Magharibi.

Amesema, "Tumekuwa tukitoa miito kwa pande zote, ikiwa ni pamoja na Israel, kuheshimu sheria za kimataifa za binadamu.”

Ameongeza kuwa, Ulaya haiwezi kuficha wasiwasi wao linapokuja suala la kinachoendelea katika Ukingo wa Magharibi na kwamba wanaunga mkono kurejea nyumbani kwa Wapalestina waliopoteza makaazi yao huko  Gaza.