![](http://eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/news/2025/02/11/raila.jpg?itok=LiqX035J×tamp=1739256289)
Kiongozi wa chama cha ODM ambaye pia ni mgombea wa wadhifa wa uenyekiti Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Raila Odinga ameonyesha utayarifu wake kuelekea uchaguzi huo zikiwa zimesalia siku 4 pekee.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa ODM ulioandaliwa katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi jana Jumatatu, Odinga amesema kwamba kujitokeza kwake kuwania kulitokana na msukumo kutoka kwa viongozi wa Afrika.
Odinga amesema kwamba alishawishiwa na baadhi ya viongozi wa Afrika kuwania wadhifa wa uenyekiti wa AUC kwani walimuona kama suluhisho bora kwa matatizo ya bara hili.
“Viongozi wa Afrika waliniambia wananitaka katika Afrika, Afrika iko na shida nyingi zaidi. Wakasema shida ambayo mko nayo Kenya ndio iko Nigeria, Ghana na kwingineko. Kwa hivyo ukija hapa juu tupate suluhisho tutaliweka katika nchi zote za Afrika.”
“Wakaniuliza, ‘kubali uje uwe kama kiongozi wa bara la Afrika’. Nikapiga moyo konde nikajiuliza na Kenya je? Nikasema Kenya iko ndani ya Afrika nan iko tayari kujaribu.”
Odinga amesema ni kutokana na msukumo huo ndio maana ametoka na kukutana na viongozi wote na kusema kwamba kama watakubali basi atakuwa mwenyekiti wa AUC.
Kiongozi huyo wa muda mrefu katika siasa za Kenya pia amesema kwamba hana wasiwasi wowote katika matokeo ya aina yoyote, akibainisha kwamba yuko tayari kwa lolote.
“Kwa hiyo mimi nimetoka nimeongea na viongozi wote wa bara la Afrika, wakikubali nitakuwa mwenyekiti wa AU.”
“Kura itapigwa Jumamosi hii inayokuja, mimi naenda, nikichaguliwa sawa na nisipochaguliwa sawa. Sivyo? Si mimi niko na nyumbani kwetu?” Odinga amesema.
Raila atachuana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Richard Randriamandrato.
Wadadisi wanasema tishio kubwa la Raila ni mgombeaji wa Djibouti, ambaye anaaminika kuungwa mkono na nchi za Kiislamu na Kiarabu