Jumatatu , 25th Nov , 2024

Wananchi wa Mtaa wa Kanoni Mburahati jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kupunguza gharama za vipimo ikiwezekana iwe bure ili waweze kujua Afya zao mapema, wapate matibabu ili kuepukana na vifo vinavyotokana na kuchelewa kupata huduma.

Rozina mathias, mkazi wa Mburahati

Wakiongea na EATV, wanasema watu wengi hawana utaratibu wa kupima afya zao ndio maana hufika hospitali wakiwa na hali mbaya kukiwa tayari na usugu wa Magonjwa.
“Sio wote tunakingana katika maisha watu wanashindwa kufanya vipimo, asilimia kubwa ya Watanzania ni wa kipato cha chini ndio maana tunaomba huduma ya vipimo Vya magonjwa iwe bure ili tujue matatizo mapema”, Exavery Jeremia-Mkazi wa Mburahati.

“Mtu unaweza ukajisahau ukajiona uko sawa kumbe una matatizo lakini kutokana na Hali ya kiuchumi unashindwa kupima Afya yako”, Rozina Mathias-Mkazi wa Mburahati.
“Wengi tumekuwa na ratiba ya kupima mpaka kuwe na changamoto mfano uume au usikie una maumivu sehemu fulani ndio unasema naenda Hospitali lakini inapotokea zoezi Kama hili tunajitokeza na kujua Afya zetu unajua hapa nilipo naendeleaje Kama kuna tatizo lolote unashughulika nalo”, Ramadhan Saidi-Mkazi wa Mburahati.

Mratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza wilaya ya Ubungo, Dokta Ilona Elisante, anasema magonjwa ya Sukari na Shinikizo la Damu yamekuwa tishio wilayani Ubungo.
“Katika mfululizo wa Magonjwa kisukari ni namba nne, pressure ni namba tatu kwahiyo tunaweza kusema bado tuna kazi kubwa ya kufanya, kwa sababu yamekuwa ni janga na vimeleta vifo vingi Vya umri kati ya miaka30-70, 75% ya vifo vinavyotokea kwa sababu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwahiyo tukiweza kuwafikia vizuri kwa mapema wananchi na wakachukua Basi tutaepukana na vifo hivyo”, Dkt. Ilona Elisante-Mratibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza Manispaa ya Ubungo.

Kuna uhuhimu gani wa wananchi kujua afya zao mapema?
“Haja yetu yote wakijua Afya zao mapema kabla hajaaanza kuumwa, viashiria vinapokuwa vinaanza wavitambue na Kama ikiwezekana wachukue hatua mapema na wote watakaogunduliwa tunawaambia waende vituo Vya Afya vya karibu na wale wanaokubali kufatiliwa watasaini kidogo ili tuweze kupima kipindi cha ufatiliaji”,  Dkt Mashombo Mkamba-Meneja mradi huduma za Afya ngazi ya jamii.