Jumatano , 13th Nov , 2024

Kutokana na kuongezeka kwa tatizo la uzazi nchini, imeelezwa kuwa mwamko wa wanaume umeongezeka kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ya uzazi huku wengine wakiweka sababu ya kuzalisha sehemu tofauti kunasababisha kutojihusisha na changamoto ya uzazi kwenye familia.

Dorry William, Tabibu wa uzazi

Hayo yamesemwa na tabibu wa maswala ya uzazi Dorry William, wakati anaongea na EATV, kuhusu onezeko la familia zinazolilia watoto.
"Wanaume wanakuja sana na mfumo wa sasa hivi wa wanaume umekuwa ni changamoto kubwa, sema jamii zetu na dhana na waafrika kwa ujumla wengi wanaamini wanawake ndio wana shida pamoja na dhana ambayo mwanamke akichelewa kupata ujauzito kuwa ana changamoto basi mwanamke ndio ana shida lakin ukweli ni kwamba kwa asilimia kubwa sasa hivi tunapokea wanaume kwa 45%", Dorry William, Tabibu wa uzazi.

Aidha anafafanua sababu mbazo zinapelekea changamoto za uzazi kwenye familia nyingi.
"Changamoto kubwa ni lifestyles imekuwa sehemu kubwa sana, lakini pia watu wanatakiwa wajue wanawake wana changamoto nyingi sana kwenye mfumo wa uzazi nikiongea hivi wanawake wananielewa, kwa sababu unaweza kukuta leo anaingia period tarehe 3, mwezi ujao 11, hii yote ni mvurugano wa homoni ambao unatakiwa kwanza urekebishwe ndipo aanze kutafuta mtoto", Dorry William, Tabibu wa uzazi.

Nao wanaume wanaelezea sababu ambazo zinapelekea wanawake wengi kulaumiwa kutoshika ujauzito.
"Wanaume wengi waoga kupima kwa sababu utakuta ana mwanamke mwingine amemwambia ana mtoto wake halafu mke wa ndani hajazaa anaogopa kwenda hospitali kwa maana anaweza kuvumbua vilivyojificha", Said Salim, Mkazi wa Dar es Salaam.

"Utakuta mtu umezaa njee kwa mchepuko lakini mke wa ndani hajazaa Wengi wanatoka nje na wanaambiwa wana watoto ndio maana mke wa ndani akishindwa kuzaa wanadhani tatizo lipo kwa mke wake kwa sababu mchepuko ana mtoto", Salehe Nasoro, Mkazi wa Dar es Salaam.

"Familia zetu za Kiswahili ndio huwa zina dhana potofu lakini jambo hili linatakiwa kliwe la pande zote ili liweze kutatuliwa", Atanas Komba, Mkazi wa Dar es Salaam.

Kuhusu matumizi ya dawa za kuzuia mimba maarufu kama P2, ambazo zimetajwa kama chanzo cha kusababisha tatizo la uzazi kwa wanawake, baadhi ya mabinti wanaelezea kwanini wengi wamekuwa wakitumia dawa hizo.
"Wengi ni tamaa wanajikuta wanataka vitu lakini kushika ujauzito hawapo tayari mwisho wa siku ndio wanaingia kwenye matumizi ya P2 ili wasishike ujauzito", Saum Msonse,Mkazi wa Dar es Salaam.

"Kwa sababu wadada wengi hawataki kushika ujauzito kabla malengo yao hayajatimia", ANASTAZIA ANDREA-Mkazi wa Dar es Salaam.

Inashauriwa familia inapopitia changamoto ya uzzi ni vema ikafika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ili ziweze kupata matibabu sahihi ya tatizo litakalogundulika.