Alhamisi , 19th Sep , 2024

Serikali imesema kwamba jumla ya vijiji 279 kati ya vijiji 306 mkoani Kigoma tayari vimeunganishwa na nishati ya umeme na kusisitiza kuwa safari ya kupeleka umeme katika vitongoji imeanza na kwamba jumla ya shilingi bilioni 100 zimetumika kupeleka umeme katika vijiji vilivyopo mkoani humo

Hayo yamebainishwa mkoani Kigoma Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu wakati wa ziara ya bodi hiyo kukagua utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kupeleka umeme vijijini.

"Zaidi ya vitongoji 595 wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme, katika vitongoji 1849 katika Mkoa wa Kigoma, vitongoji zaidi ya 1370 tayari vimeshapata umeme, tunaendelea kuhamasisha wananchi kuendelea kutumia miradi hii kutekeleza na kubuni shughuli za kiuchumi zitakazoweza kuboresha uchumi wao pamoja na kulinda miradi hii maana serikali imewekeza fedha nyingi sana," amesema Mhandisi Saidy.

Wakati wa ziara hiyo, Balozi Meja Jenerali (mstaafu) Kingu amewataka wakandarasi kuhakikisha wanamaliza miradi hiyo kwa wakati na muda uliopangwa, na kwamba hawatasita kuwachukulia hatua za kimkataba mkandarasi yoyote atakayeshindwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kama inavyotakiwa.

"Tumeshatoa maelekezo, hakuna muda wa nyongeza utakaotolewa kwa mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza mradi wake ndani ya muda uliopangwa, labda kwa sababu maalum, tumewaelekeza wakandarasi pia wahakikishe material yote yanayohitajika kama nguzo kabla ya msimu wa mvua kuanza ili miradi hiyo isichelewe kama ilivyo dhamira ya serikali umeme kuwafikia wananchi wote ndani ya muda," amesema Balozi Meja Jenerali (mstaafu) Kingu