Jumapili , 14th Jul , 2024

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb.) ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki mkoa wa Simiyu amesema kuwa amefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika jimbo hilo katika sekta za afya, elimu,maji,umeme na barabara.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanslaus Nyongo

Nyongo ambaye yuko kwenye ziara katika jimbo hilo kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo amesema hayo kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kata ya Nghwigwa,Mwamanenge,Senani na Ipililo akihutubia mikutano hadhara na kukagua miradi hiyo.

Amesema kuwa kwa kipindi cha miaka takribani minne tangu achaguliwe kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa awamu ya pili, Serikalini imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema serikali  imeleta fedha hizo katika jimbo hilo kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na shule za sekondari,Vituo vya afya, Miradi ya Maji,Miundombinu ya barabara na Umeme.

Amesema kuwa katika sekta ya afya wameweza kuwa na zahanati na  vituo vya afya ambavyo vinawahudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo.

 Amesema kuwa katika miradi ya maji baadhi ya vijiji vilivyoko katika Jimbo hilo vitapata maji ya Ziwa Victoria ili kuondoa tatizo la maji pindi mradi huo ambao tayari umeanza kutekelezwa katika mkoa wa Simiyu.

Pia ameongeza kuwa katika jimbo hilo vijiji vyote na taasisi zote za serikali zimepatiwa huduma za nishati ya umeme ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo muhimu kwa maisha ya kila siku na sasa kila kitongoji kitapatiwa umeme.

Kwa upande wa barabara amesema kuwa barabara zilizo nyingi katika mji wa Maswa zimewekewa lami pamoja na taa za barabarani na kwa sasa nguvu amezielekeza katika barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini(TARURA) hasa maeneo ya vijijini ambazo zilizo nyingi zimeharibiwa kwa kiasi kikubwa cha mvua zilizonyesha ambapo kwa musimu uliopita zilikuwa ni nyingi karibu Nchi nzima.