Ijumaa , 3rd Mei , 2024

Mwananmke mmoja ambaye amefahamika kwa jina la Evarine Paul mkazi wa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera amefanyiwa upasuaji wa tumbo katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita na kuondolewa uvimbe wenye kilo tano ambao amedumu nao kwa kipindi cha miaka kumi.

Madaktari Bingwa wa Mama Samia Wakiendelea na Upasuaji

Upasuaji huo umefanywa na kambi ya madaktari bingwa wa Mama Samia waliopo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita huku mama huyo akisema amezunguka sehemu mbalimbali kutafuta matibabu bila mafanikio.

“Uvimbe wangu ulikuwa na miaka kama kumi nilianzia Biharamuro ikashindikana na  nimeenda Mwanza hospitali nikarudishwa ndo nikaja hapa Geita kwa msichana wangu hapa ndo juzi akawa amenileta, nilipofika hapa nikapata huduma nzuri ninashukuru kwakweli nikawa nimetolewa ule uvimbe na sasa naendelea vizuri” Evarine Paul, aliyefanyiwa upasuaji

Mratibu wa huduma za kibingwa kutoka wizara ya afya Dkt John Mwombeki amesema zoezi la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wanachi zitaendelea kufanyika kila mwaka.

“Wakati serikali ikiwainaendelea na jitihada za kuhakikisha kila hospitali ya mkoa wa inakuwa na madaktari bingwa sasa tunaendelea na kambi yetu ili kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi ili kuwapunguzia adha ya kwenda mwendo mrefu kufuata huduma hizo hospitali za kanda au Taifa”Dkt John Mwombeki, Mratibu wa huduma za kibingwa wizara ya afya

Hospitali ya Rufaa mkoa wa Geita imepokea madaktari bingwa 29 ambapo hadi kufikia sasa zaidi ya watu 1000 wamepatiwa huduma.