
Wakaguzi kutoka Shirikisho la soka barani Afrika CAF wamefanya ziara kwenye viwanja vya Tanzania vitakavyotumika kwenye Mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa Ligi za ndani CHAN inayotarajia kufanyika mnamo Septemba 2024.
Akizungumza na EATV , Kaimu Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo hapa nchini Ally Mayay amesema miongoni mwa viwanja vilivyokaguliwa ni uwanja uliopo nyuma ya uwanja wa Benjamin Mkapa, uwanja wa chuo cha polisi Kurasini, pamoja na ule wa Gymkhana uliopo Posta
"Baada ya kufika hapa walikagua viwanja vya mazoezi ambavyo vitaendana hadhi ya CAF kila timu inatakiwa ifanye mazoezi kwenye uwanja unaoendana na uwanja wa mchezo bahati nzuri Jeshi la Polisi limetupa ushirikiano mkubwa tuufanyie ukarabati uwanja wa Kurasini, amesema Mayayi.
Kwa upande mwingine,Ally Mayay amesema maandalizi yanaendelea vyema kuelekea kwenye mashindano hayo ambayo itakuwa kipimo cha kuonyesha ushindani na kudai Tanzania itafanya vizuri kutokana na ushindani uliopo kwa kila mchezaji hapa nchini.