Alhamisi , 15th Feb , 2024

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 23 za Tanzania Bara ambapo kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani jijini Dodoma leo tarehe 15 Februari, 2023.

“Fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia tarehe 26 Februari, 2024 hadi tarehe 04 Machi, 2024, na uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 04 Machi, 2024, kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 05 hadi 19 Machi, 2024 na uchaguzi utafanyika tarehe 20 Machi, 2024,” imesema taarifa hiyo. 

Taarifa hiyo imeanisha kuwa uchaguzi huo umetangazwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, akiitaarifu kuhusu uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika kata 23 za Tanzania Bara. 

Imeongeza kuwa Waziri ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kata zinazohusika na uchaguzi huo mdogo ni pamoja na Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Mji Kibaha), Fukayosi  (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea). 

Nyingine ni  Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa),   Mshikamano (Halmashauri ya Wilaya ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Nkokwa (Halmashauri ya Wilaya ya Kyela), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).