Alhamisi , 25th Jan , 2024

Mabomba ya ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Ohima Nchini Uganda hadi Chongoleani jijini Tanga yamewasili nchini kwajili ya kujenga kilomita 600 kwenda kwenye kituo kikubwa cha kuchemshia mafuta kitakachojengwa Nzega

Naibu waziri Mkuu na waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko ametoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea eneo la Chongoleani jijini Tanga mahala ambapo panajengwa matanki makubwa ya kuhifadhia mafuta ghafi kutoka nchini Uganda. 

"Kwa ujumla asilimia 32 ya ujenzi imekwishakufikiwa na mabomba yanaendelea kuja kwajili ys kujenga kilomita 600 kwenda Nzega mkandarasi pamoja na EACOP wameendelea kusimamiwa vizuri na mamlaka za serikali, "alisema Dkt Biteko. 

"Wito wetu mkubwa kwanza wa ujenzi tunataka tuone kampuni nyingi zaidi za watanzania zinapewa kazi kwenye mradi huu kwenye ajira watanzania wengi zaidi wapewe kazi na hata wale wachache wanaokuja kama wataalamu ni muhimu kuangalia uwiano wa namna wanavyolipwa kwasababu unaweza kukuta mtaalamu mmoja analipwa pengine mshahara wa watanzania 50 jambo hilo haliwezi kuwa sawa hivyo ni muhimu kuangalia kada ambazo zinapatikana ndani watanzania walipwe, "alisisitiza Dkt. Biteko. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba ameishukuru Kampuni ya bomba la mafuta ghafi la Afrika mashariki (EACOP)  kwa kuutekeza mradi huo bila kikwazo chochte ambapo amewahakikishia kuwa serikali ya Mkoa Tanga itaendelea kushirikiana nao ili kuufanikisha mradi huo. 

"Tunawashukuru wenzetu wa Eacop mpaka sasa wameonyesha ni raia wema wameendelea kuishi miongoni mwetu hapa Tanga hatujapata matukio yeyote ya kuleta taharuki hivyo niwahakikishie wenzetu wa Eacop kwamba serikali ya Mkoa Tanga tuko pamoja na wao, "alibainisha Kindamba. 

Mara baada ya kutoka eneo la Chongoleani mahala ambapo ndio kitovu cha mradi wa bomba la mafuta,  ziara ya Naibu waziri Mkuu Dkt Dotto ilitembelea Bohari ya kuhifadhia mafuta ya GBP iliyopo Jijini Tanga na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha mazingira rafiki kwa wawekezaji nchini huku Mwakishi wa Mkurugenzi wa GBP akisema Kampuni hiyo inaipongeza serikali ya awamuya sita kwa kuboresha sekta ya kibiashara. 

"GBP tunaipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais mahiri mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan na tunaunga mkono jitihada zinazofanywa za kuboresha sekta ya kibiashara,  kuimarisha uchumi na diplomasia sambamba na uchumi imara " alisisitiza Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa GBP. 

Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2025 na kwamba baada ya mafuta ghafi kupokelewa  kwenye kituo hich  yataanza kusafirishwa kupelekwa kwenye  maeneo mbalimbali duniani.