Jumapili , 24th Dec , 2023

Watu nane wamefariki dunia akiwemo mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu na wengine sita kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Probox iliyogongana na gari ya kampuni ya ujenzi ya barabara ya Chiko katika eneo la barabara ya Kibondo-Kakonko mkoani Kigoma, ambapo chanzo cha

ajali hiyo kimetajwa kuwa ni uzembe wa dereva wa gari ndogo pamoja na mwendokasi.
 

Akizungumza leo Desemba 24, 2023 na waandishi wa habari kuhusiana na ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, amesema ajali hiyo imetokea jana Jumamosi majira ya saa 11:30 jioni katika Kijiji cha Mumkungwa, Kata ya Misenzero, barabara ya Kibondo-Kakonko.

Waliofariki kwenye ajali hiyo wametajwa kuwa ni pamoja na dereva wa gari ndogo, Hamisi Chaurembo (27), Bernadina Reuben  (22), Madua Asukile, Ntiganiza Bihezako (67), Vedastus Paul (28), Vladmir Vedastus (1) marehemu wengine ambao majina yao hayajatambuliwa hadi sasa.

Andengenye amesema majeruhi hao wapo katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa matibabu na baada ya uchunguzi majeruhi watatu kati ya sita waliopata ajali wameumia zaidi hivyo watapewa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando iliyopo mkoani Mwanza na wengine watatu wanaendelea na matibabu hospitalini hapo.