Alhamisi , 21st Dec , 2023

Jeshi la Polisi Kamisheni ya Polisi jamii ngazi ya mkoa wa Arusha imekuja na mbinu ya kukabiliana na uhalifu katika mkoa huo ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini kwa kushirikisha makampuni binafsi katika kukabiliana na uhalifu.

Akiongea katika kikao na viongozi wa makampuni ya ulinzi mkoani humo Mkuu wa Polisi Jamii mkoani humo ACP Peter Lusesa amesema polisi wanao wajibu wa kisheria wa kulinda raia na mali zao huku akibainisha kuwa makampuni binafsi ya ulinzi yamesajiliwa kwa kazi ya ulinzi na kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi.

Ameongeza kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura amefanya maboresho makubwa ya kiutendaji ndani ya Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kuboresha mafunzo ya kitaaluma lengo likiwa ni kuwajengea uwezo maafisa wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali katika utendaji wa kisasa na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Pia amesema siku za hivi karibuni walikwenda katika nchi ya China kujifunza namna bora ya ulinzi katika taifa hilo ambalo limeendelea katika maswala ya ulinzi huku akibainisha kuwa Taifa hilo limejikita pia katika kuwashirikisha makampuni ya ulinzi ambayo yametoa mchango mkubwa zaidi katika kukabiliana uhalifu katika Taifa hilo.

ACP Lusesa ameyataka Makampuni kuweka utaratibu  mzuri katika kuajiri askari wenye utimamu wa mwili na akili ili kupata fursa hiyo ambayo Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limepanga kutumia mbinu hiyo ya kuyatumia Makampuni ya ulinzi katika kusimamia na kufanya ulinzi kulingana na vigezo ambavyo vitawekwa na Jeshi la Polisi Mkoani humo.

Kwa upande wake James Lugangila ambaye anatoka kampuni binafsi ya ulinzi amesema yapo makampuni ambayo yanatia doa huku akiliomba Jeshi hilo ambalo ni waangalizi na wakaguzi wa makampuni hayo kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa makampuni ambayo yanafanya kazi kwa mazoea katika Mkao huo ambapo amepongeza mpango huo ambao utakwenda kusaidia kuongeza nguvu katika ulinzi Mkoani humo.