Alhamisi , 16th Nov , 2023

Wito umetolewa kwa wananchi kujitokeza kupima VVU kwa hiari na kujua hali zao ili kuendelea kuishi kwa kuzingatia matokeo, kwa wale ambao hawatakutwa na maambukizi ni nafasi kwao kuendelea kuishi ili wasiambukizwe na wale ambao watakutwa na maambukizi wana nafasi ya kuendelea kuishi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,anayeshughulika na Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama

Kauli hiyo imetolewa wakati wa kikao cha pamoja Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,anayeshughulika na Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima, kuhusu kuelekea maandalizi ya siku ya UKIMWI kitaifa, katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Ameongeza kusema tafiti zote za miaka mitano zimeonesha wanaume hawajitokezi kupima, na hawajitokezi kuanza kupata dawa, na hivyo kusumbuliwa sana na magonjwa nyemelezi yanayotokana na virusi vya UKIMWI.

"Virusi vya UKIMWI na UKIMWI upo ni wajibu wa kila mwananchi kuendelea kuchukua tahadhari," amesema Waziri Mhagama

Akizungumzia kuhusu malezi, ametoa rai kwa wazazi kukaa na familia na kuwaelimisha uwepo wa tatizo hili la UKIMWI.

Awali Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema maandalizi kuelekea wiki Maadhimisho ya siku ya UKIMWI yanaendelea vizuri

"Lengo ni kupeleka ujumbe kwa wananchi, huku tukitupia jicho kwa kundi la vijana na kwa kushiriki kwao itasaidia kupeleka ujumbe kwa vijana wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki," amesema RC Malima