Jumatatu , 13th Nov , 2023

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania Dkt Tulia Ackson, amesema kuwa jamii inapaswa kuondoa fikra potofu kwamba wanawake hawapendani na badala yake waige mfano wa Rais Samia namna anavyowapa nafasi wanawake wenzake katika nyadhifa za uongozi.

Dkt Tulia Ackson

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 13 Novemba, 2023, wakati wa hafla maalum ya kumpongeza baada ya kushinda Urais wa IPU iliyoandaliwa na Chama cha Walimu wilaya ya Mbeya Jiji.

Dkt. Tulia amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa namna alivyohakikisha Tanzania inashinda katika uchaguzi wa IPU uliofanyika mwezi Oktoba nchini Angola kwakuwa nafasi hiyo ilikuwa ni lazima nchi husika itoe ridhaa ya kutoa muwakilishi na kwa upendo wake alifanya hivyo.

Dkt. Tulia amewataka Walimu wote nchini kuendelea kuweka juhudi katika kujenga taifa lililoelimika kwa kutoa elimu iliyo bora kwa Wanafunzi kwakuwa serikali imefanya kazi kubwa kwa kuboresha mazingira ya kazi kuwa rafiki ikiwemo kulipwa madai yao mbalimbali na kwa wakati.