Jumatano , 18th Oct , 2023

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Kagera Neema Lugangira kupitia kwa mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima, amewasilisha msaada wa magodoro 20 na blanketi 50 kwa ajili ya kusaidia wananchi waliokumbwa na maafa ya mvua na upepo mkali ulioezua nyumba zao.

Baadhi ya blanketi na godoro zitakazogawiwa kwa wananchi waliopata maafa

Mvua iliyoambatana na upepo mkali imenyesha alfajiri ya leo Oktoba 18, 2023, huku zaidi ya nyumba 100 zikiezuliwa paa zake na upepo na kupelekea kifo cha mtu mmoja, ambapo wakazi wa Kata ya Rwamishenyi, Hamugembe na Kashai ndiyo wameathirika zaidi na mvua hizo.

Aidha kufuatia mvua iliyonyesha Oktoba 16 mwaka huu, zaidi ya nyumba 150 na vyumba vya madarasa 20 viliezuliwa na upepo, huku mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Karambi wilaya ya Muleba mkoani Kagera yakiathiriwa.