Jumanne , 10th Oct , 2023

Mti mkubwa ulioangushwa na upepo miezi mitano iliyopita umewashangaza watu katika wilaya ya Mbogwe mkoani Geita baada ya kuamka wenyewe na kuanza maisha yake kama kawaida.

Mti uliojinyanyua

Tukio hilo la kusitaajabisha limetokea katika Kata ya Nanda iliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita, baada ya mvua kubwa kunyesha usiku EATV imefika eneo la tukio na kuzungumza na wanafamilia wanaomiliki mti huo wanasimulia tukio lilivyokuwa.

"Niliamka asubuhi watoto wanasema mti umesimama nikasema kweli nikavaa haraka haraka na mimi kutoka nje nikaona mti umesimama kweli," amesema Samwel Somi, mmiliki wa mti

"Usiku huo kulinyesha mvua kubwa yenye upepo hatukujua sababu ni nini kuamka asubuhi tunaona mti umeamka kama unavyoona na tulivyokuwa tumeukata matawi sasa unaanza kuchipuka tena, " ameongeza mmoja wa wanafamilia hao

Kwa upande wao wananchi wa Kijiji hicho wanasema ni mara yao kwanza tukio kama hilo kutokea katika eneo lao.

"Mimi hili tukio nimelisikia ila mimi nilishuhudia kuna kipindi mvua ilinyesha mti huu ukaanguka baada ya siku nikasikia ule mti umeamka mmmh nikasema si waliukata eeh waliukata matawi lakini umeinuka na umeanza kuchipuka tena," amesema jirani

Diwani wa Kata ya Nanda Matius Lugoda akizungumza na EATV amewaomba wananchi kuwa watulivu na kuacha kuusisha tukio hilo na imani za kishirikina.