Jumanne , 10th Feb , 2015

Naibu waziri wa afya Mh. Steven Kebwe amesema serikali iko katika hatua za mwisho za kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo sugu la madaktari kukimbilia nje ya nchi kwa kisingizio cha kutafuta maslahi.

Naibu waziri wa afya nchini Tanzania Mh. Steven Kebwe.

Akizungumza jijini Arusha baada ya kukutana na wataalam wa afya wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya Bara la Afrika wanaojadili namna ya kupunguza tatizo la uhaba wa madaktari maeneo ya vijijini Dr. Kebwe amesema baada ya kubaini kuwa tatizo liko kwenye mfumo wameanza kuufanyia marekebisho ambayo kuondoka kwao kutakuwa na tija badala ya madhara

Ametaja baadhi ya marekebisho yanayoendelea kufanywa kuwa ni pamoja na uweze kuwapa nafasi wauguzi watabibu kutoa tiba zilizoko ndani ya uwezo wao ambazo kwa mfumo wa sasa zinatakiwa kutolewa na daktari licha ya kuwa ndani ya uwezo wa wauguzi.

Baadhi ya wadau wa afya akiwemo Prof Egberty Kessy na Dkt. Otilla Flaviana wamesema uchunguzi umeonesha kuwa wauguzi watabibu ndio wanaofanya kazi kubwa kuliko hata madaktari na wako karibu zaidi na wagonjwa hivyo mpango huo ukikamilika utakuwa ni ukombozi mkubwa.