Jumatatu , 5th Dec , 2022

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Khalifan Haule amehimiza wananchi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika upandaji wa miti ya matunda ili kupata matunda na vivuli katika maeneo yao

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Khalifan Haule akimwagilia maji mti wa matunda alioupada katika shule ya msingi ya Mwisengi wakati wa zoezi la upandaji wa Miti, Desemba 5, 2022 Musoma mkoa wa Mara ikiwa ni kuelekea mkutano Mkuu wa Nane wa Mwaka wa Wadau wa Lishe katika Wilaya ya Musoma Mkoani Mara

Ametoa kauli hiyo hii leo Desemba 5, 2022 wakati wa zoezi la upandaji miti ya matunda katika shule ya Msingi ya Mwisenge iliyopo mkoani Mara.Zoezi hili ni moja ya shughuli zinazoambatana na Mkutano Mkuu wa Nane wa mwaka wa Wadau wa Lishe.

Aidha jumla ya miti 300 imetolewa na kugawa katika shule sita ikiwemo; Mwisenge, Mtakuja, Nyarigamba A, Nyarigamba B, Nyabisare na Nyarugusu ambapo kila shule itapewa miti 50.

“Leo tunazindua upandaji wa miti hii kwenye shule ya Kihistoria aliyosoma Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyeyere ikiwa ni ishara ya kuunga mkono jitihada za kuhamasisha ulaji wa matunda kwa lengo la kuimarisha masuala ya lishe nchini,”aslisema Dkt. Haule

Aidha lengo la zoezi hilo ni kuimarisha utekelezaji wa masuala ya  lishe nchini kwa kuhamasisha ulaji wa matunda na mbogamboga katika jamii zetu.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe nchini Dkt.Germana Leyna amesema taasisi yake imejithatiti kuhakikisha elimu ya masuala ya chakula na lishe bora inatolewa kwa makundi yote ikiwemo watoto waliopo mashuleni.

Aliongezea kuwa watu wengi wanakula kwa mazoea na si kula lishe bora hivyo jamii haina budi kubadilisha mitazamo juu ya masuala ya lishe na kuyapa kipaumbele.

"Hakuna mtu anayeweza kufanikiwa ikiwa anachamoto za kiafya zinazochangiwa na lishe duni, hivyo kila mmoja anajukumu la kuzingatia lishe bora kwa afya bora,"alisisitiza Dkt. Germana

Alitoa neno la Shukrani Mstahiki Meya wa Manispaa la Musoma Kapteni Mstaafu Patrick Gumbo alipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe pamoja na Mkoa kwa kuratibu zoezi hilo huku akitoa rai kwa kila shule kuhakikisha wanatunza miti hiyo ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

"Ni jambo jema limefanyika leo, jukumu lililopo mbele yetu ni kuhakikisha miti inatunzwa na inaleta manufaa kama ilivyokusudiwa," alisema Patrick

Naye Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Sigawa Mwita alitoa shukrani kwa kuitumia shule hiyo yenye historia kubwa nchini kwa kuzingatia Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisoma hapo na kueleza zoezi hilo ni sehemu ya kumuenzi mwalimu kwa kuzingatia alikuwa kinara wa masuala ya upandaji wa miti.

"Shule yetu inajumuisha na wanafunzi wenye mahitaji maalum na imendelea kuwa na ufaulu mzuri sana hii imetupa hamasa na kuonesha mnajali na mnatambua mchango wa shule hii," alisema Mwalimu Mwita