
Yohana Samweli - Mkulima
Utekelezaji huo unaogharimu zaidi ya Bilioni 58 kwa mwaka wa fedha 2022-2023 umeendelea kufanyika kwa kuboresha na kuanzisha miundombinu mbalimbali ya umwagiliaji kwa maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Skimu ya Mawala iliyopo Kahe wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro imepongezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya umwagiliaji Raymond Mndolwa kwa maendeleo na utunzaji wa mradi huo wakati akikagua maendeleo ya mradi huo na kushauri kutengwa eneo maalum kwa ajili ya Serikali kujenga ghala la wakulima hao kuhifadhi mazao.
Wakulima katika skimu hiyo wameipongeza serikali kupitia Mh.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji inayowawezesha kulima kwa uhakika na kuwa na uhakika wa wa chakula bila kutegemea misimu ya mvua.
Kwa upande wake Mjumbe wa Skimu hiyo Mariam Sadiki Mashambo ametoa wito kwa wakulima wanaonufaika na kilimo cha umwagiliaji kuchangia ada za maji ili kutunza na kukarabati miundombinu hiyo iliyojengwa na serikali na kuifanya idumu kwa muda mrefu na kuhudumia wakulima wengi zaidi.
Mpango wa serikali ifikapo mwaka 2025 ni kuwafanya wakulima hapa nchini kuacha kulima kwa kutegemea mvua na badala yake walime kwa miundombinu ya umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa mavuno.