Jumatatu , 11th Apr , 2022

Waziri wa Fedha na Mipango nchini Dr Mwigulu Nchemba amewataka watanzania kuendelea kufanya shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi ili kukabiliana na majanga mbalimbali ambayo yanaikumba dunia kwa sasa.

Waziri Nchemba ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ili kukabiliana na hali ya kupanda kwa bei ya bidhaa nchini ambapo amewataka watanzania kuacha kulaumu kwani hakuna uzembe uliosababisha tatizo hilo.

“Janga likishatokea sio wakati wa kulaumiana kwa sababu si janga la kibinadamu, si jambo la uzembe wa kisera, sisi kama watanzania tunapaswa kuhakikisha tunaendelea na shughuli za uzalishaji kuweza kulinda uchumi wan chi yetu” amesema Nchemba.

Waziri huyo amesema zipo hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kupambana na kupanda kwa bei ya bidhaa nchini huku akisema kuwa tatizo hilo sio la Tanzania pekee hivyo njia zinazochukuliwa zinaangalia pia soko la dunia la bidhaa husika.

Ametaja baadhi ya hatua zinazochukuliwa na serikali kuwa ni kupunguza mafuta yanayotumika kwenye magari, bidhaa zinazohusu usafirishaji, Kupunguza Rate ya kodi kwa asilimia 10 katika sukari iliyoagizwa kwa sasa nje ya nchi.

Kuhusu Mafuta ya kula amesema serikali imeielekeza TRA waangalie nini kinaweza kufanyika na kuangalia viwango vipya vitakavyoruhusu kupunguza gharama inayohusu makato ili kuja na viwango vipya vya kodi

Aidha amesema Mafuta ya magari (petrol na dizeli Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuangalia tena gharama na kuona kiwango kinachoweza kuleta unafuu kwa wananchi.

Katika mkutano huo Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji amesema Serikali imeanzisha mfumo wa upatikanaji wa bei za bidhaa wa kila siku na kuanzisha namba maalumu  itakayowekwa hadharani ambapo wananchi watapiga simu wanapoona mabadiliko ya bei.