Wakazi wa kijiji cha Ayalabe kata ya Ganako wilaya ya Karatu wameiomba serikali isikie kilio chao kwa kuchukua hatua kwa watendaji wa halmashauri waliohusika katika kuuza hekari 30 za ardhi ya shule ya msingi Ayalabe pamoja na kuuza mlima pekee wa kijiji kwa mwekezaji huku wakigawana zaidi ya shilingi milioni 500 za chama cha ushirika cha kijiji hicho bila kuwashirikisha wananchi.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika kijiji cha Ayalabe watu hao walionekana kuwa na jazba wamesema matendo mengi ya kifisadi yanafanyika katika kijiji hicho bila kuwahusisha na wanapo uliza wanatishiwa kufunguliwa mashitaka.
Wamesema wamelalamika katika ngazi mbalimbali bila mafanikio na kinachowauma zaidi ni kuuzwa kwa mlima Ayalabe kwa wawekezaji na sasa wanaiomba serikali kuingilia kati vinginevyo watafanya maamuzi yaliyo ndani ya uwezo wao.
Katika mkutano huo alitokea mmoja wa wananchi ambaye alitaka kutetea watendaji wanaolalamikiwa lakini wananchi walimjia juu na kutaka aache kuongea hali iliyotaka kusababisha mkutano uvunjike na mwenyekiti wa mkutano alilazimika kumkatisha mtu huyo.
Akizungumzia malamiko hayo mbunge wa Karatu mchungaji Israel Natse amesema yeye kama mmoja wa viongozi wa halmashauri hiyo hakutarajia kukutana na mambo mazito kiasi hicho.
Amesema sehemu kubwa ya mgogoro huo unatokana na viongozi kutojali miiko ya uongozi lakini kwa kiwango cha ufisadi huo hatoweza kufumbia macho kilio hicho na anakipeleka katika ngazi za juu na kinachohushu wananchama wa chama chake atapeleka katika mkutano mkuu wa CHADEMA.