
Kocha msaidizi wa Simba, Selemeni Matola akiongea mbele ya Wanahabari baaada ya mchezo wa jana dhidi ya Dodoma Jiji.
Matola ameyasema hayo alipokuwa anaongea na wanahabari usiku wa jana kwenye dimba la Mkapa akitoa tathmini yake ya kiufundi juu ya kiwango cha timu chake hususani kwenye kipindi cha kwanza ambapo mpaka mchezo unaenda mapumziko matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Matola amesema, “Nafikiri hata hii michezo iliyofululiza kidogo imechangia uchovu, wachezaji kipindi cha kwanza hawakuweza kufunguka zaidi angalau kipindi cha pili lakini yote kwa yote tunamshukuru Mungu kwa kupata alama tatu ambazo tulizihitaji”.
Na baada ya kusema hayo akagusia kuelekea kwenye mchezo wake unaofuata dhidi ya Kagera Sukari wa hatua ya mtoano ya 16 bora ya michuano ya kombe la Shirikisho nchini utakaochezwa Mei mosi 2021 saa 1:00 usiku kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Malengo yetu sisi ni kama tulivyofanya msimu uliopita, tutetee ubingwa wa FA na hatimaye ubingwa wa ligi. Hatutokuwa na msihara katika mchezo huo tutaingia na mziki wote kuhakikisha unatetea ubingwa wa kikombe hiki, nia yetu sisi ni tuchukue vikombe viwili ”
“Tunahitaji kwenda kutetea FA na hakuna jinsi ya kutetea lazima tumfunge Kagera Sukari hapa katika mchezo unaokuja” Matola akamalizia.
Baada ya ushindi wa usiku wa jana, Simba imesalia kileleni mwa VPL wakiwa na alama 61 utofauti wa alama 4 na watani wake Yanga ambao wamewazidi Simba kwa michezo miwili, Simba akiwa na michezo 25 ilhali Yanga akiwa amecheza michezo 27.