Afisa Uhusiano wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Rajab Mwenda.
Mpango wa Taifa wa Damu Salama nchini Tanzania umesema bado uchangiaji wa damu nchini haukidhi mahitaji ya wagonjwa katika hospitali na vituo mbalimbali vya afya nchini.
Akiongea jijini Dar es Salaam Afisa Uhusiano wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Rajab Mwenda amesema mahitaji ni wastani wa chupa kati ya laki nne na laki tano kwa mwaka huku mpango ukikusanya chupa 140,000 hadi 160,000 kwa mwaka ambapo pia kuna changamoto ya tatizo la uuzaji damu.
Mwenda amesema uuzaji wa damu unaofanywa na watumishi wa afya wasio waaminifu umekuwa sababu kubwa ya kufifisha ari ya wananchi kuchangia damu katika mikoa mbalimbali nchini.
Wakati huo huo, watu watano wanashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani Manyara nchini Tanzania kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mifugo na mapigano yaliyohusisha wakulima na wafugaji wilayani Kiteto ambayo yamesababisha mauaji ya watu wanne Walayani humo.
Akitoa tamko la serikali leo Bungeni Mjini Dodoma Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe. Mathias Chikawe amesema eneo hilo kwa sasa ni tulivu ingawa hali bado ni tete, lakini jeshi la polisi linaendelea kudhibiti hali ya usalama katika eneo hilo.
Mhe. Chikawe amewataka wakazi wa wilaya ya Kiteto kuwa watulivu wakati serikali inalishughulikia suala hilo na kuwataka viongozi wa kisiasa kuchukua hatua za kuhakikisha usuluhishi wa kudumu unapatikana katika eneo hilo.