Alhamisi , 1st Oct , 2020

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, amemtaka mgombea urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu, kuripoti kituo cha Polisi Moshi Kilimanjaro, kutokana na kitendo anachodaiwa kufanya cha kukaripia, kuwagombeza na kugombana na viongozi wa polisi.

Kushoto ni mgombea urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu na kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro.

IGP Sirro amesema hayo leo Oktoba Mosi, 2020, na kusema kuwa hata kabla ya kutoa agizo hilo, alizungumza na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, kukaa na watu wake wazungumze suala la utii wa sheria bila shuruti.

"Nimeona matukio kadhaa yanafanyika na viongozi wa CHADEMA wamekuwa na tabia ya kukaripia na kuwagombeza Askari Polisi, tumeona mara kadhaa Tundu Lissu anagombana na viongozi wa polisi nimuombe sana anayoyafanya watanzania wenye hekima na wazalendo wanayaona", amesema IGP Sirro.

Aidha IGP Sirro aneongeza kuwa, "Lissu hayuko juu ya sheria, polisi tukiamua kutimiza wajibu wetu asilalamike na chama chake, vyama viko karibu 12 jeshi la polisi limepewa wajibu wa kulinda watu na mali zao, yeye hana uwezo wowote wa kupambana na jeshi la polisi isifike mahali akaona ana kiburi cha kupambana na polisi, niwaombe CHADEMA hii tabia iishe".