Madini ya Tanzanite ambayo yamepatikana Mererani Arusha
Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa migodi ya madini ya Tanzanite katika eneo la mji mdogo wa Merelani yaliyopo wilayani simanjiro mkoani manyara, mchimbaji mdogo wa madini hayo Laizer Kuryani, amefanikiwa kupata mawe mawili makubwa na yenye uzito mkubwa, katika historia ya uchimbaji wa Tanzanite.
Serikali kupitia benki kuu imeyanunua mawe hayo yote mawili moja likiwa na uzito wa kilo tisa nukta mbili saba na jingine likiwa na uzito wa kilo tano kwa gharama ya takribani shilingi bilioni nane za kitanzania.
Jiwe la kwanza la madini hayo limebainika kuwa na thamani ya shilingi 4,368,649,470.08 na la pili likiwa na thamani ya shilingi 3,375,503,233.74 na kwa kutambua unyeti wa madini hayo waziri wa madini Dotto Biteko ameamuru madini hayo yote yanunuliwe na serikali kwa haraka.
Kwa upande wao baadhi ya wachimbaji wadogo wa Madini ya Tanzanite katika migodi ya Merelani akiwemo Laizer mwenyewe wamepongeza kuwepo kwa ukuta katika eneo la Merelani na pengine ndio chimbuko la kuonekana kwa madini yenye ukubwa wa aina hiyo.