Jumatano , 13th Feb , 2019

Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba amefunguka kwamba amepata ajali baada ya gari alilokuwa amepanda kugonga punda aliyekuwa akikatisha barabarani.

Kushoto ni picha ya gari ya Mbunge Mwigulu Nchemba aliyopata nayo ajali.

Akizungumzamapema leo na vyombo vya habari katika hospitali ya Mkapa jijini Dodoma anakopatiwa matibabu, Mwigulu amesema alikuwa akitokea mkoani Iringa kuelekea mkoani  Singida kuhudhuria kikao cha kamati ya siasa.

“Nilikuwa siangalii mbele kwa kuwa nilikuwa naongea na simu lakini ghafla nilishtushwa na tahadhari ya ajali niliyopewa na dareva wangu,” amesema Mwigulu.

“Nilipotazama mbele niliwaona punda watatu wanakatisha barabara na mmoja alifanikiwa kuvuka na kuwagonga wengine wawili. Nilichosikia ni sauti ya kishindo kikubwa kilichoashiria kuwa tumepata ajali, namshukuru Mungu ni mwema kwa kuwa ametuepusha na kifo". Amesema Mwigulu wakati akizungumza na vyombo vya habari.

Amesema baada ya hapo aliona moshi umetanda ndani ya gari hali iliyoashiria gari hilo lingeweza kulipuka lakini wasamaria wema walifika na kuwaokoa na kuwawahisha hospitali ya Benjamin Mkapa.

Mapema asubuhi ya leo taarifa za Mwigulu Nchemba kupata ajali zilisambaa huku chanzo kikiwa hakijatajwa mpaka pale alipozungumza mwenyewe.