Alhamisi , 20th Dec , 2018

Tasnia ya filamu duniani imekuwa ikiangaliwa  kwa jicho kubwa zaidi na wasanii, huku kati ya wasanii wengi wanaotoka barani Afrika, wachache ndio wanaofanikiwa kupenya na kuingia kwenye kiwanda maarufu cha filamu Marekani, Hollywood.

Lupita Nyong'o

Hapa nakuletea orodha ya waigizaji wa kike ambao wana asili ya Afrika, wanaofanya vizuri Hollywood, na kuepeperusha bendera ya nchi zao ipasavyo.

Wasanii hao wanaweza wakawa ni wa kuzaliwa hapa Afrika, au wazazi wao ni wa Afrika lakni walihamia ughaibuni kwa sababu mbali mbali.

Lupita Nyong'o

Ni mtoto wa Prof. Anyang' Nyong'o wa nchini Kenya, aliyewahi kuishi Mexico ambako ndiko alikozaliwa Lupita Nyong'o na kupata elimu yake. Lupita alipata umaarufu mkubwa baada ya kushiriki kwenye filamu ya '12 years a slave', na kufungua milango zaidi ndani ya Hollywood, ambapo baadaye alifanikiwa kuingia kwenye studio za Marvel na kushiriki filamu mbali mbali ikiwemo Black Panter ambayo ilimng'arisha zaidi duniani.
 

Charlize Theron

Alizaliwa Afrika Kusini na kukulia huko. Alianza sanaa kama mwanamitindo na baadaye alihamia jijini New York, ambako alikutana na 'casting agents', baada ya hapo alipata dili la kuigiza kwenye filamu mbalimbali nchini humo ikiwemo 'devils advocate' na nyinginezo ndani ya Hollywood.

Benu Mabhena

Akizaliwa nchini Zimbabwe kwa wazazi wa Kindebele na Zulu. Mabhena aliishi maisha yake nchi mbalimbali barani Afrika na Uingereza, wazazi wake walipokuwa wakitafuta hifadhi ya kisiasa, na hatimaye kufanikiwa kuweka makazi rasmi nchini Marekani. Mabhena ameigiza kama mke wa Djimon Hounsou kwenye filamu ya 'Blood Diamond' ambayo ilimpa umaarufu zaidi licha ya kuwa kwenye filamu nyingine nyingi.

Chipo Chung

Alizaliwa jijini Dar es salaam nchini Tanzania kwa wazazi mchanganyiko wenye asili ya Kichina na Zimbabwe. Chipo aliishi kwenye kambi za wakimbizi nchi nyingi za Afrika ikiwemo Msumbiji na Zimbabwe, na kufanikiwa kusoma katika chuo cha sanaa cha Yale cha nchini Marekani, ambacho kilifungua milango zaidi ya sanaa yake na kupata dili ya kuigiza filamu ya 'sun shine', 'in the loop' na nyinginezo.

Liya Kebede

Mwenye uzuri wa kuvutia wa Ethiopia, Liya alianza sanaa yake kama mwanamitindo hadi kufikia kutajwa na jarida la forbes kuwa miongoni mwa wanamitindo bora wa kike wanaolipwa pesa nyingi zaidi mwaka 2007. Alipogeukia uigizaji, Liya ameshashirikishwa kwenye filamu kama 'Lord of War', 'The best offer', ambazo zimemfanya azidi kung'ara Hollywood.

Rachel mwanza

Licha ya kuathiriwa na vita nyumbani kwao nchini Congo, Mwanza ni mmoja kati ya watoto nyota wanaokua kwenye kiwanda cha Hollywood, baada ya kuonekana kwenye filamu ya 'rebele, war watch', ambayo ilivutia watu wengi kutokana na umahiri wake wa kuigiza.  Hivi sasa binti huyo amepata ufadhili wa masomo akiendeleza kiwango chake cha elimu ambayo alilazimika kuikosa kutokana na vita iliyokuwa ikiendela nchini Congo.

Leleti Khumalo

Akizaliwa nchini Afrika Kusini. Leleti alijizolea umaarufu mkubwa duniani hususani barani Afrika, baada ya kuigiza filamu ya Sarafina, ambayo aliicheza kwa ustadi mkubwa na kusisimua wengi, wakielezea maisha halisi ya vijana wa Afrika Kusini wakati wa vitendo vya ubaguzi wa rangi. Pia Leleti ameshaonekana kwenye filamu ya Hotel Rwanda, ambayo nayo ilileta hamasa kubwa sana Afrika ikisimulia jinsi mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 yalivyotokea na jinsi yalivyoathiri nchi ya Rwanda.

Carmen Elizabeth Ejogo

Ingawa ni raia wa Uingereza, Carmen ni Mwafrika kutokana na baba yake kuwa na hasili ya Nigeria, na mama yake ni Mscotish. Alianza kuigiza akiwa nchini Uingereza na baadaye kuhamia Marekani, ambako aliendelea sanaa yake na kupata fursa ya kuigiza kwneye filamu kubwa kama The Brave one, The Avengers kulifanya jina la muigizaji huyo lizidi kupaa kwenye chungu cha Hollywood.

Danai Gurila

Akiwa mtoto wa mwanakemia kutoka Zimbabwe, alizaliwa huko Iowa Marekani ambako baba yake alikuwa akifundisha somo la Kemia, alisoma sanaa, jambo ambalo limekuja kumlipa kwenye maisha yake kwani ameweza kuigiza kwenye filamu zilizovunja rekodi Hollywood kama 'The Walking Dead' na Black Panther.

Sophie Okonedo

Baba yake akiwa ni Mnigeria na mama ni Myahudi, Sophie ana uraia wa Uingereza. Amefanikiwa kukaa kwenye ramani ya Hollywood kwa kuigiza kwenye filamu ya Hotel Rwanda, When the Nature Call na nyinginezo.