Jumanne , 18th Dec , 2018

Baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wake wa jana Jijini Mwanza, kocha mkuu wa klabu ya Mbao FC, Amri Said ameibuka hadharani na kumkataa kocha wake msaidizi, Ally Bushiri kwa madai ya kutokuwa na maelewano mazuri.

Kocha Amri Said

Kocha mkuu Amri Said amesema kuwa endapo uongozi utaendelea kumbakiza kocha huyo msaidizi klabuni hapo, yuko radhi yeye aondoke amuache kocha huyo aendelee na kazi.

Akizungumza baada ya kupata matokeo katika mchezo huo ambao klabu ya Mbao iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC, kocha mkuu, Amri Said amesema, "mwanzoni sikuonekena kwenye mchezo kwasababu nilikwenda hospitali kwaajili ya jino, suala la mwalimu msaidizi mimi naona ni suala la vyombo vya habari tuu. Uongozi waliponifuata niliwaambia sikubaliani na hilo kwasababu walipanga bila kukaa na mimi".

"Mwalimu Ally Bushiri ana leseni B na mimi nina leseni B, sasa hapo nani atakuwa mkuu na nani msaidizi, hapo mimi naona ni vitu vya kiunafiki tuu na majungu majungu. Ingelikuwa hata mimi nisingekubali kufanya kazi na mwalimu mwenye leseni B kama yangu," ameongeza.

Aidha, kocha Amri Said amesema kuwa aliwapa ushauri uongozi wa Mbao kumtafuta kocha mwenye leseni A ili naye apate kujifunza au mwenye leseni C lakini viongozi walipuuzia mawazo yake na kusisitiza kuwa kwa sasa morali yake kwenye timu imeshuka tofauti na mwanzo.

Baada ya matokeo ya jana, Mbao FC imefikisha pointi 24 katika nafasi ya nne nyuma ya Simba yenye pointi 27 katika nafasi ya tatu, Azam FC iliyopo nafasi ya pili kwa pointi 40 na kinara Yanga yenye pointi 44.