Jumatatu , 10th Dec , 2018

Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera ameitaja siri anayoitumia kwa wachezaji wake ndani ya vyumba vya kubadilisha nguo ambayo inapelekea kuwapa ushindi mfululizo katika ligi.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera

Yanga ilitokea nyuma na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa tano mfululizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara TPL kwa kuichapa Biashara United mabao 2-1 katika uwanja wa taifa, mabao yaliyofungwa na mlinzi, Abdallah Shaibu 'Ninja' na mshambuliaji Heritier Makambo, huku bao pekee la Biashara United likifungwa na Abdulmajid Mangalo.

Akizungumzia juu ya siri ya kupata matokeo mazuri katika mchezo huo, kocha Mwinyi Zahera amesema, "wachezaji wangu walijitoa na kufanya vitu vizuri, ila tu walikosa bahati. Tulishambulia sana tukakosa bahati, kwenye mapumziko nikawaambia kwamba "mliona mechi na Prisons tulivyofanya?, kipindi cha kwanza tulifungwa bao moja lakini mwisho matokeo yalikuwaje? 3-1 na hapa fanyeni hivyo", na ndiyo maana tukaibuka na ushindi".

Pia kocha huyo amezungumzia juu ya taarifa kuwa anawasema vibaya wachezaji wake katika mikutano na waandishi wa habari, ambapo amesema,"watu wanafikiri kuwa ninavyowasema wachezaji wangu hapa ninawaonea au wanakasirika hapana, mimi ninasema ukweli, hata Makambo nilivyomsema kuwa akiendelea mambo yake nitamtoa kikosini alisikia na akabadilika".

Kwa ushindi huo, sasa Yanga inarejea kileleni ikiwa na jumla ya pointi 41 na kuwaacha wapinzani wao Simba kwa tofauti ya alama 14 ambao wana michezo mitatu mkononi ili kuwa sawa kimichezo na Yanga. Nafasi ya pili inashikiliwa na Azam FC yenye alama 39 katika michezo 15 iliyocheza.