Jumatano , 19th Sep , 2018

Kiungo wa klabu ya Singida United, Godfrey Mwashiuya amekiri kuwa klabu yake ya zamani ya Yanga iliwahi kumbania kwenye dili mbalimbali za kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Kiungo wa Singida United, Godfrey Mwashiuya.

Mchezaji huyo ambaye aliichezea Yanga kwa takribani misimu mitatu, amejiunga na Singida United msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga na kutojumuishwa katika mipango ya kocha Mwinyi Zahera.

Akizungumza na, East Africa Radio kuhusiana na sababu zinazopelekea wachezaji wengi wanaocheza katika klabu kubwa za Simba na Yanga kubweteka,  Mwashiuya amesema,

 Ni kweli hilo lipo lakini cha pili ni kwamba viongozi wetu hawakai karibu na wachezaji ndio maana vipaji vingi vinapotea, kiongozi anapokuwa karibu na mchezaji na anapopata fursa akamkubalia ni vizuri ”.

Mfano, mimi nilishawahi kupata fursa nyingi za kwenda nje ikiwemo klabu ya TP Mazembe pamoja na nchi za Morocco na Comoro, mimi nilikuwa tayari lakini viongozi wakanikatalia wakasema mimi bado mtoto mdogo wanahitaji kunitumia. Kwahiyo ni kitu ambacho mimi kilinirudisha nyuma ”, ameongea Mwashiuya.

Mchezaji huyo mzaliwa wa wilaya ya Mbozi mkoani Songwe alianzia soka lake katika mashindano ya UMISETA ambapo kupitia mashindano hayo alipata nafasi ya kusoma shule ya sekondari ya Makongo.

Baada ya kutofanikiwa kusonga mbele kimasomo alijiunga na klabu ya Kimondo ya mkoani Mbeya ambayo alicheza kwa kiwango kikubwa na kuivutia klabu ya Yanga na kumsajili. Aliitumikia Yanga kwa misimu mitatu na kufunga mabao mawili pekee na kusajiliwa na Singida United ambayo anaichezea hadi hivi sasa.