Ijumaa , 17th Aug , 2018

Kuelekea kuanza kwa fainali ya michuano ya Kikapu nchini ya Sprite Bball Kings, timu mbili zilizotinga hatua hiyo Mchenga Bball Stars na Flying Dribblers, zimeonekana kuviziana zikisubiri kutambuana kwa mbinu kwenye game 1.

Kushoto ni nahodha wa Mchenga Mohamed Yusuf na kulia ni nahodha wa Flying Dribblers Habirmana Mayeye.

Wakiongelea 'game 1' kati ya 'best of five' ambayo itapigwa kesho Agosti 18, 2018 kwenye uwanja wa taifa wa ndani manahodha wa timu hizo, Mohamed Yusuf wa Mchenga na Habirmana Mayeye wa Flying Dribblers, wamesema wanachoweza kuahidi ni ushindani tu na mchezo ndio utaamua mshindi.

''Unajua hii ni game iliyojirudia baada ya msimu uliopita Mchenga kututoa katika hatua ya nusu fainali na hiyo ilitokana na wachezaji wetu wengi kuondoka baada ya robo fainali lakini mwaka huu tupo kamili kwahiyo tutatoa ushindani kwa bingwa mtetezi na dakika zenyewe zitaamua'', amesema Mayeye.

Kwa upande wake Mohamed amesema wao kama mabingwa watetezi wanachoweza kuwapa mashabiki ni kuendelea kuwa washindani tu kwani kabla ya ushindi huwa wanawaza namna ya kushindana na wanapoweza matokeo huwa yanakuja yenyewe.

Fainali hizo zitapigwa kwa mtindo wa 'best of five' na mshindi atajinyakulia kombe na shilingi milioni 10 huku mshindi wa pili akijipatia milioni 3 na MVP ataondoka na milioni 2. Usikose kesho kwenye uwanja wa taifa wa ndani kutakuwa na burudani nyingi na vinywaji baridi vya Sprite ambao ndio wadhamini wa michuano hii.