Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba nchini Tanzania, Deus Kibamba.
Tamko la kutaka kusitishwa kwa mchakato huo limetolewa jijini Dar es Salaam leo na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Deus Kibamba, ambaye ameitaka serikali pia kusitisha uchaguzi wa serikali za mitaa uliokuwa ufanyike baadaye mwaka huu kwa sababu hizo hizo pamoja na kutokwepo kwa muda wa kutosha kwa ajili ya maandalizi.
Kibamba amesema ni busara pekee ndio itakayounusuru mchakato huo, ambapo hakusita kulaumu namna wanasiasa walivyouteka mchakato huo na kuonekana kuwa wa kisiasa zaidi badala ya kubeba ajenda na hoja zinazohusu maslahi mapana ya wananchi.
Kauli ya Kibamba imekuja wakati ambapo wajumbe kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA kusisitiza kuwa hautohudhuria vikao vya bunge hilo vinavyotarajiwa kuendelea mapemba mwezi ujao, kwa madai kuwa mchakato huo umetekwa na wajumbe kutoka chama tawala CCM ambao wameacha kujadili rasimu na vipengele vinavyohusu maslahi ya pande zote.
Hapo jana, wajumbe kutoka UKAWA walisusia kuhudhuria mkutano wa kujadili hatma ya mchakato wa katiba mpya ulioitishwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba Samuel Sitta, kwa madai kuwa mwenyekiti huyo hana nguvu ya kimaadili ya kuitisha mkutano huo kutokana na yeye mwenyewe kuwa sehemu ya walalamikiwa.