Jumatano , 15th Feb , 2017

Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete, amefunguka kuhusu sakata la dawa za kulevya na kuipongeza serikali hususani Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kwa kuanzisha vita hiyo na kutaka wahusika wachukuliwe hatua.

Mh. Ridhiwan Kikwete akiwa ndani ya Studio za EA Radio

Kikwete amefunguka hayo leo katika kipindi cha East Africa Breakfast cha EA Radio, kinachoruka kila siku saa 11:00 alfajiri hadi saa 3:00 asubuhi.

Ametumia nafasi hiyo kuishauri serikali kuifikisha mwisho vita hiyo, ili kulimaliza kabisa tatizo hilo kwa kuwa limepoteza vijana wengi wenye uwezo mkubwa na mchango katika taifa, huku akitolea mfano uwezo wa msanii wa Bongo Fleva, Langa ambaye kwa sasa ni marehemu ikidaiwa kuwa alipoteza maisha kutokana na dawa hizo, pamoja na shida alizokuwa akizipata msanii Ray C, za kutafuta dawa hizo hata usiku wa manane.

Ameitaka mamlaka mpya wa dawa za kulevya kuwachunguza watu 97 ambao majina yake yamekabidhiwa hivi karibuni na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, na yeyote atakayethibitika kuhusika, achukuliwe hatua, huku akionesha imani kubwa kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt Rogers William Sianga.

Msikilize hapa alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na Songa wa Songa, wa East Africa Breakfast........................

 

 

Ridhiwan Kikwete - Mbunge wa Chalinze