Jumatatu , 30th Jan , 2017

Mwenyekiti wa CCM Mbeya Mjini, Efrahim Mwaitenda mwenye umri wa miaka 60 amejeruhiwa kwa kupigwa risasi mgongoni na mtu au watu wasiofahamika.

Mwenyekiti wa CCM Mbeya Mjini (Aliyekaa) akipeleka hospitali)

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 29.01.2017 majira ya saa 05:45 usiku katika kitongoji cha Ilopa, Kijiji cha Mahenge, Kata ya Makwale, Tarafa ya Ntebela, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya.

Amesema tukio hilo limetokea wakati akiwa amelala kitandani nyumbani kwake Ntembela ambapo mbinu iliyotumika ilikuwa ni  kukata wavu wa dirisha na kumjeruhi kwa kutumia silaha za kienyeji zinazotumia risasi za gololi.

Mwenyekiti huyo amefikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na hali yake inaendelea vizuri.

Lukula amewaambia waandishi wa habari kuwa nia ya shambulizi hilo ilikuwa ni kutaka kuumua na kwamba juhudi za kuwatafuta na kuwakamata wahusika zinaendelea.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dk. Godlove Mbwaji amekiri kumpokea mgonjwa huyo akisema kuwa Mwaitenda amepigwa risasi mgogoni ambayo imemjeruhi vibaya na kuwa madaktari bingwa wanaendelea kumtibu na kuondoa vipande vya risasi mwilini.

Naye Kaimu Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Zongo Lobe Zongo amelishukuru jeshi la polisi kwa kuchukua hatua za haraka kushughulikia tukio hilo, huku mkuu wa wilaya ya Mbeya William Ntinika akilitaka jeshi la polisi kuwasaka watu waliofanya tukio hilo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.