Baadhi ya vijana waliojitokeza katika dimba la Lake Tanganyika mjini Kigoma
Huo ni mwendelezo wa programu hiyo ya kusaka vijana nyota kutoka maeneo mbalimbali nchini, watakaounda timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya timu hiyo.
Mahudhurio katika mkoa huo yalikuwa makubwa kutokana na jumla ya vijana 544 kufanyiwa usaili na benchi la ufundi la timu ya vijana ya Azam FC chini ya Mwingereza Tom Legg, anayesimamia mradi huo.
Legg anayeshirikiana kwa ukaribu na kocha mzawa kijana, John Matambara, alihitimisha zoezi hilo kwa kuchagua vijana sita bora na wengine 20 akiwaweka kwenye kumbukumbu yake kwa ajili ya kuwapa nafasi nyingine baadaye.
Takwimu zinaonyesha kuwa mpaka sasa katika mikoa yote saba ambayo imetembelewa, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro & Dodoma, Mbeya, Mwanza, Visiwani Zanzibar na Kigoma, Azam FC imefanikiwa kuwafanyia usaili jumla ya vijana 3,809 huku waliochaguliwa wakiwa ni 89 tu na wengine 171 wakiorodheshwa kwenye kumbukumbu ya mradi huo.
Vijana wote ambao wamechaguliwa kwenye mikoa iliyotembelewa, baadaye mwezi huu wanatarajia kuitwa katika Makao Makuu ya Azam FC ‘Azam Complex’ kwa ajili ya hatua ya fainali, ambayo ndiyo itatoa wachezaji bora watakaounda kikosi hicho kinachotafutwa, ambacho kitaanza kupewa mafunzo kuanzia Januari mwakani.