Alhamisi , 17th Nov , 2016

Wahitimu wa mafunzo mbalimbali ya mchezo wa kuogelea nchini wametakiwa kutumia elimu na ujuzi walioupata katika jamii ili kupata vipaji vingi zaidi katika mchezo huo.

Baadhi ya makocha waliopata mafunzo

 

Akizungumza na Hotmix Michezo wakati wa kufunga kozi ya kitaifa ya mchezo wa kuogelea, Noel Kihunsi akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea nchini TSA , Ramadhani Namkomveka, amewataka wahitimu hao kushirikiana na wanachama wa mchezo huo walio katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuweza kusambaza mchezo huo.

Kozi hiyo iliyoendeshwa kwa siku 10 na Mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Kuogelea (FINA), Joshua Neuloh kutoka nchini Ujerumani imeshirikisha walimu 30 kutoka mikoa ya Arusha, Singida, Dar es Salaam, Zanzibar, Singida na Mwanza.

Aliongeza kusema kuwa ni kazi ngumu kupata mafunzo hayo kupitia kwa Olympic Solidarity, kwani kuna vyama 27 nchini, ambavyo ni wanachama wa TOC vyote vikihitaji kupatiwa msaada huo.

Ramadhani Namkoveka - Katibu Mkuu TSA

Mwaka 2008 TSA ilipata mafunzo mengine ya makocha wa mchezo huo, ambapo jumla ya washiriki 30 walihudhuria huku 25 wakiwa wanaume na wanawake watano.

Naye makamu mwenyekiti wa TSA, Thauriya Diria aliishukuru Olympic Solidarity kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kuwapatia mafunzo hayo ya ngazi ya juu ya kuogelea.