Alhamisi , 10th Nov , 2016

Serikali imezitaka halmashauri nchini kujenga vyumba vya upasuaji na maabara katika vituo vya afya ili iweze kupeleka wahudumu wengi wa afya katika maeneo yao ili kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinavyotokea wakati wa kujifungua.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangalla.

 

Akijibu swali bungeni mjini Dodoma hii leo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangalla amekiri kuwa tatizo la vifo vya wajawazito na watoto ni kubwa nchini hususan katika maeneo ya vijijini kutokana na kukosa huduma za upasuaji wa dharura na wakupanga.

Dkt. Kigwangalla amesema pamoja na hayo serikali inaendelea kutekeleza mpango mkakati wa kuvijengea uwezo vituo vya afya hasa vilivyopo vijijini ili viweze kutoa huduma ya upasuaji hasa wa dharura.

Aidha, Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuboresha miundombinu, watumishi, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kuokoa maisha ya akina mama wengi walio vijijini.