Jumanne , 8th Nov , 2016

Jumla ya madereva 62 wanaoendesha mabasi yaendayo haraka (UDART) wamechukuliwa hatua za kinidhamu kwa sababu ya kukiuka sheria za barabarani.

Basi la mwendo wa haraka

 

Idadi hiyo ya madereva imetajwa leo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kiembe Samaki Mhe. Ibrahim Mohammed lililohoji kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali juu ya madereva hao ambao hawafuati sheria za barabarani.

Mhe. Jafo amekiri kuwa madereva hao wamekuwa wakiendesha mabasi hayo kwa kasi kubwa kiasi cha kuhatarisha maisha ya watu waendao kwa miguu lakini madereva hao wanapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani kama ilivyo kwa madereva wanaoendesha aina nyingine ya magari.

Selemani jafo - Naibu Waziri TAMISEMI

“Tangu mabasi haya yaanze kutoa huduma, tumeshawachukulia hatua za kinidhamu madereva 62 ambapo kati ya hao, madereva 20 wamepewa onyo kwa makosa ya usalama barabarani, wawili wamefukuzwa kazi na madereva 40 wamekatwa mishahara yao kwa makosa mbalimbali ya barabarani”, alisema Mhe. Jafo.

Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa kwa sasa mabasi hayo yamefungwa vifaa maalum kwa ajili ya kutoa ishara ya dereva anayezidisha mwendo wa zaidi ya Kilomita 50 kwa saa moja ili kudhibiti mwendo mbaya wa mabasi hayo.