Ijumaa , 4th Nov , 2016

East Africa Television LTD ambao ndiyo waandaaji wa EATV AWARDS, mwishoni mwa wiki hii wanatarajia kuanza kutangaza wasanii wanaowania tuzo hizo katika vipengele mbalimbali ambao wamepitishwa na timu ya majaji pamoja na 'Academy' maalum ya tuzo hizo.

 

Wasanii hao katika vipengele hivyo ambavyo vipo 10 huku kimoja kati yake kikiwa ni cha tuzo maalum, wataanza kutangazwa siku ya Jumapili ya tarehe 6 Novemba 2016 hadi tarehe 9 Novemba 2016.

Siku ya tarehe 6 Novemba wasanii watakaotangazwa ni kutoka katika vipengele viwili pekee, ambavyo ni muigizaji bora wa kiume na msanii bora chipukizi, ambapo kila kipengele kitabeba majina matano ya washiriki ambao watapigiwa kura na wananchi.

Baada ya hapo vipengele vingine vitafuata kwa siku nyingine tofauti tofauti mpaka kufikia tarehe 9 Novemba, na kisha mchakato wa kuanza kupigiwa kura utafuata.

EATV AWARDS ndizo tuzo za kwanza Afrika Mashariki kushirikisha wasanii wa nchi zote tatu za Afrika Mashariki, huku wasanii wa filamu na muziki wakishiriki moja kwa moja, na zinatarajia kufikia kilele chake tarehe 10 Desemba 2016

Tags: