Ijumaa , 28th Oct , 2016

Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Vincent Mashinji amewataka wananchi kutumia fedha kwa umakini kwa kubana bajeti ya matumizi yao ili kuhakikisha wanaweza kumudu hali ya maisha kwa sasa.

Dkt. Vincent Mashinji

 

Akijibu maswali ya wananchi waliotaka maoni yake kuhusu hali ya maisha kwa sasa kupitia KIKAANGONI kinachorushwa na EATV, Dkt. Mashinji amewataka watanzania kuhakikisha wanatumia fedha  vizuri kwa sababu hali ya uchumi siyo nzuri kwa wananchi wa kawaida.

“Watanzania wenzangu tutumie fedha vizuri, hali ni ngumu na ni ngumu kwa sababu ajira nazo hazipo hadi makampuni binafsi yanakusudia kupunguza watu, hivyo tujipange vizuri chini ya uongozi wa awamu hii ya tano, na hali itazidi kuwa ngumu zaidi” Amesema Dkt. Mashinji.

Amesema jambo pekee linaloweza kurudisha nchi katika hali ya kawaida na wananchi wakawa na maisha mazuri, ni kwa Rais Magufuli, kurudi nyuma na kufanya mashauriano na wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya upinzani juu ya nini cha kufanya huku akimtaka pia kukubali ushauri badala ya kwenda na mwelekeo anaokwenda nao sasa.

Aidha Mashinji ameongeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira nchini CHADEMA imejipanga kupitia Baraza la Vijana kuanza mkakati maalumu wa kuwafundisha vijana ujasiriamali ili waondokane na dhana ya kuajiriwa wajiajiri wenyewe.