Alhamisi , 25th Aug , 2016

Kituo cha sheria na haki za binadamu nchini LHRC kimeishauri serikali kulinda na kuheshimu haki za binadamu kama zilivyoainishwa kwenye Katiba ya Tanzania na sheria za nchi kama walivyoapa kuzilinda kwenye kiapo chao cha utii na uongozi.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Dkt. Hellen Kijo-Bisimba

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Dkt. Hellen Kijo-Bisimba wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya haki za kiraia na kisiasa zilivyo kwa sasa nchini.

Dkt. Kijo-Bisimba amesema vyombo vya dola na viongozi wa serikali hususani Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa weledi, kufuata sheria na taratibu zake bila kuwatisha na kuwajengea hofu wananchi.

Amesema vyama vya siasa nchini vishindane kwa hoja na kuacha kutumia vyombo vya dola katika kushinikiza hoja au matakwa yao, na kwamba hali hiyo itasaidia kukuza na kuimarisha haki za binadamu na democrasia nchini na kuleta usawa na ushindi wa kweli.

Amesema kushindana kwa hoja pia ni fursa kwa wananchi na watanzania kusikia, kuelewa na kupambanua hoja na kujenga jamii yenye uelewa na upeo mpana kuhusu masuala yanayowahusu ya ndani na nje ya nchi.

Amesema Msajili wa vyama vya siasa asimamie katika nafasi yake ya mratibu, msimamizi na mbeba bendera ya maendeleo ya vyama vya siasa na ukuaji wa democrasia na kutojiingiza katika kuonekana kuegemea upande au chama chochote ili kusaidia kujenga mshikamano wa taifa na uimarishaji wa democrasia na vyama vya siasa.

Kwa upande wa tume wa haki za binadamu na utawala bora Dkt Bisimba ameishauri iendelee kusimamia haki za binadamu na kuishauri serikali na mamlaka zake kila mara kuhusu heshima na ulinzi wa haki za binadamu nchini.

Pia ametaka mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya urudishwe na kuendelezwa ili kupata katiba bora itakayoanzisha vyombo huru na mifano imara ya uwajibikaji ili kusaidia ulinzi wa haki za binadamu, demokrasia na uwepo wa maendeleo endelevu.