Jumatatu , 1st Aug , 2016

Zaidi ya asilimia 97 ya Wanawake nchini wanawanyonyesha watoto bila kufuata utaratibu na ushauri wa wataalam wa afya hivyo kuhatarisha afya za watoto wao.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi Msaidizi wa Lishe wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Georgina Msemo wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani.

Dk. Msemo amesema, asilimia 59% ya watoto wenye umri kuanzia mwezi 0 hadi miezi 6 wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee ikimaanisha kuwa asilimia 41 ya watoto wapo hatarini kupata Utapiamlo.

“Kina mama asilimia 97 wananyonyesha watoto wao lakini ni wengi miongoni mwao awawanyonyeshi ipasavyo jambo ambalo linahatarisha afya ya watoto” amesema.

Kutokana na tatizo hilo ameitaka serikali, makampuni na taasisi binafsi na waajiri wote nchini kuhakikisha kuwa mama anaye nyonyesha anapewa muda kulingana na sheria inavyoagiza ya kunyonyesha watoto wao kulingana na taratibu za kisheria zilizowekwa na serikali.

Dkt. Msemo amesema ili kulinda maisha ya mtoto jitihada zifanyike kuhakikisha kuwa mama anapunguziwa kazi ili aweze kunyonyesha ipasavyo, kulinda usambazaji holela wa vyakula vya watoto wachanga na wadogo.

Kila mwaka Agost 1 mpaka 7 Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto kwa lengo la kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji na ulishaji bora wa watoto.