Mcheza Golf wa Ireland, Rory Mcllroy amejiondoa kwenye mashindano ya Olimpiki, huko Rio, Brazil, mwezi Agosti mwaka huu, kwa sababu ya tishio la ugonjwa wa virusi vya Zika.
Ugonjwa wa Zika unaosababishwa na mbu, unaathiri ubongo kwa watoto na kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo, na tayari shirika la Afya duniani WHO limezuia wajawazito kusafiri kwenye mji wa Rio, nchini Brazil.
Mcllroy mwenye umri wa miaka 27, alinukuliwa mwezi uliopita akisema kuwa yeye na mchumba wake Erica Stroll, wanafikiria kuwa na mtoto kipindi kifupi kijacho, hivyo tamko lake la leo la kutoshiriki Olimpiki ni kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Zika, baada ya kutafakari sana.
Kamati ya Olimpiki ya Ireland, imesema imesikitishwa kujitoa kwa Mcllroy, lakini inaheshimu maamuzi yake.
Kujitoa kwa Mcllroy, ni pigo kwenye Olimpiki, baada ya mchezo huo wa golf kurudishwa kwenye mashindano hayo, kwa mara ya kwanza baada ya kukosekana kwa miaka 112.

